Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, katika hafla iliyoandaliwa na taasisi ya “Panda Mti wa Mzeituni” (Stichting Plant een Olijfboom) katika uwanja wa Markt, uliopo katikati ya mji wa Den Bosch nchini Uholanzi, kumbukumbu ya watoto na waandishi wa habari wa Kipalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza iliadhimishwa.
Katika hafla hiyo, picha na majina ya waandishi wa habari waliouawa katika mashambulizi ya Israel viliwekwa hadharani katika uwanja huo. Vilevile, maelfu ya jozi za viatu vya watoto ziliwekwa hapo ikiwa kama kumbukumbu ya watoto waliopoteza maisha yao.
Wakati wa programu hiyo, majina ya watoto waliouawa huko Ghaza pamoja na umri wao walipofariki yalikuwa yakisomwa moja baada ya jengine na washiriki mbalimbali.
Pia, watu wa kujitolea waliokuwepo katika hafla hiyo waligawa vipeperushi kuhusu hali ya Ghaza ili kuwafahamisha wapita njia kuhusu maendeleo na mazingira yanayoendelea katika eneo hilo.
Inawezekanaje Kuzungumzia Usitishaji wa Vita?
Bi. Esther van der Most, mkurugenzi wa taasisi ya “Panda Mti wa Mzeituni”, katika mahojiano na mwandishi wa Anadolu alisema kwamba; taasisi hiyo imeandaa kwa mara ya kumi na saba hafla ya kumbukumbu ya watoto wa Kipalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel, na kwa mara ya tano hafla ya kumbukumbu ya waandishi wa habari waliouawa.
Akieleza kwamba; katika hafla ya kwanza ya kumbukumbu iliyofanyika mwezi Desemba mwaka 2023 katika mji wa Rotterdam, jozi 8,000 za viatu vya watoto zilioneshwa, alisema: “Leo idadi ya watoto waliouawa imefikia 21,000. Tuko hapa leo kwa sababu tunataka Wapalestina waweze kuishi, wafikie umri mkubwa, wawe salama na waishi kwa uhuru, lakini kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina, jambo hilo kwa sasa haliwezekani.”
Van der Most alisisitiza kwamba; mauaji hayo ya kimbari hayaishii Ghaza pekee, bali yanaendelea pia katika Ukingo wa Magharibi, na akaongeza: “Wakati watu wanauawa kila siku, inawezekanaje kuzungumzia usitishaji wa vita? Wiki iliyopita mtoto wa miezi saba aitwaye Sam aliuawa katika Ukingo wa Magharibi. Hakuwa mtoto wa kwanza; katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mamia ya watoto wengine pia wamepoteza maisha yao huko, hali hii lazima ikomeshwe.”
Aidha, akiihutubia serikali ya Uholanzi, alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za vitendo na kusema: “Komesheni hali hii, wekeni vikwazo na chukueni hatua, msiipe Israel nafasi ya kipekee wakati inaendelea kuangamiza taifa zima, nina hasira na serikali yangu, kwa sababu hatupaswi kushirikiana na utawala wa Israel ambao unaliangamiza taifa zima.”
Mkurugenzi wa taasisi ya “Panda Mti wa Mzeituni” pia alieleza kwamba; sambamba na watoto wa Kipalestina, waandishi wa habari waliouawa walipewa heshima katika hafla hiyo na kusema: “Idadi ya waandishi wa habari waliouawa sasa imevuka watu 300. Unapozima sauti za waandishi wa habari, kwa hakika unataka kuzuia ukweli usiwafikie wananchi, lakini sisi tutaendelea kuufikisha ukweli.”
Maoni yako